Maofisa saba wa Jeshi la Polisi nchini wanaotuhumiwa kwa mauaji ya mfanyabiashara wa madini Musa Hamisi (25) mkoani Mtwara, wamefikishwa mahakamani leo ikiwa ni kwa mara ya tano.
Hata hivyo Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Hakimu mkazi Mtwara, Lugano Kasebele ameahirisha kesi hiyo hadi Apriil 8 mwaka huu kutokana na upelelezi kutokamilika.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 25 mwaka huu kwa shtaka la mauaji ya mfanyabiashara huyo wa madini aliyekuwa mkazi wa kijiji cha Ruponda mkoani Lindi.
Maofisa hao saba wa Jeshi la Polisi nchini wanaoshtakiwa kwa mauaji ni aliyekuwa Mkuu wa upelelezi wilaya ya Mtwara, Gilbert Kalanje, aliyekuwa mkuu wa kituo cha polisi Mtwara, Charles Onyango, aliyekuwa Mkuu wa intelijensia mkoa wa Mtwara Nicholaus Kisinza, Mkaguzi wa polisi John Msuya, Mkaguzi msaidizci wa polisi, Marco Mbuta, Mkaguzi wa polisi Shirazi Mkupa na Koplo Salum Mbalu.