Simba: Hatukupanda basi, ni ‘shuttle’

0
1202

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amekanusha taarifa kwamba walipanda basi baada ya kufika nchini Benin kama ambavyo imezushwa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii.

Akizungumza na TBC Taifa leo amesema kuwa walikuwa kwenye basi maalum (shuttle) lililokuwa likiwatoa ndani ya uwanja wa ndege baada kutua.

Akizungumzia mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya ASEC Mimosas, amesema kwamba lengo lao ni kushinda mchezo huo kesho na kufuzu hatua ya robo fainali lakini pia wanataka kushinda ili iwe zawadi kwa Rais Samia Suluhu kutimiza mwaka mmoja.

Katika mchezo wa awali uliopigwa Dar es Salaam, Tanzania, Simba iliibuka na ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya ASEC Mimosas ambayo imeshinda michezo miwili iliyocheza nyumbani.

Simba SC inaongoza Kundi D ikiwa na alama 7 baada ya kushuka dimbani mara nne, huku wenyeji wao wakiwa nafasi ya pili na alama 6 baada ya michezo minne.

Mchezo huo utakaoanza majira ya saa 1:00 Jioni kwa saa za Afrika Mashariki utatangazwa moja kwa moja na TBC Taifa na kurushwa kwenye ukurasa wa YouTube wa TBCOnline.