Makamu wa Rais ahimiza utunzaji wa mazingira

0
202

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango leo Machi 18, 2022 ametembelea na kukagua Shamba la Miti katika Msitu wa Rubare na maporomoko ya maji Kyamunene yaliopo Bukoba mkoani Kagera.

Akiwa katika Msitu huo Makamu wa Rais amewataka viongozi wa mkoa wa Kagera kuendelea kuhamasisha wananchi kupanda miti, kwani msitu huo una mchango mkubwa kwa vyanzo vya maji vya mkoa huo hivyo ni muhimu kulindwa dhidi ya uharibifu wa mazingira.

Ameuasa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kutoa elimu na utaalamu wa vijana wanaojishughulisha na shughuli hizo katika halmashauri zote nchini ili waweze kuendeleza ujuzi huo kwa wengine na kuchangia katika uhifadhi.

Aidha, amesema ipo haja ya kuanza kuwatumia kikamilifu wanafunzi tangu wakiwa wadogo katika masuala ya uhifadhi wa mazingira ikiwemo kuwapa elimu pamoja na motisha za kutembelea vivutio vya utalii vya kimazingira wakati wanapofanya vizuri darasani.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais katika shamba hilo, Mkuu wa Uhifadhi Mandalo Salum amesema uanzishwaji wa shamba hilo umelenga kulinda vyanzo vya maji pamoja na mmomonyoko wa udongo ambapo katika msitu wa Rubare wenye jumla ya Hekta 6374 upandaji miti umefanyika katika hekta 2551 huku zinazobaki zikitumika kulinda vyanzo vya maji.

Mandalo amesema shamba hilo limekuwa likichangia mapato ya serikali kuu kupitia uuzaji wa miti pamoja na kutoa asilimia tano ya mapato yake kwa serikali za mitaa.