Mahakama yampa siku 21 Makonda kujibu hoja

0
169

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, jijini Dar es Salaam imetoa siku 21 kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwasilisha hati kinzani dhidi ya maombi yaliyofunguliwa mwandishi wa habari Saed Kubenea, kutaka kibali cha kumfungulia kesi ya jinai.

Amri hiyo imetolewa na Hakimu mkazi wa mahakama hiyo Aron Lyamuya, baada ya Wakili wa Makonda Goodchance Reginald kuwasilisha maombi ya kuongezewa muda wa kujibu hoja za mawakili wa Kubenea ukiongozwa na Hekima Mwasipu kwa madai kuwa mteja wake hakupata hati ya wito wa mahakama.

Hata hivyo Wakili wa Kubenea, Hekima Mwasipu amepinga hoja za Wakili huyo akidai kuwa hajaeileza mahakama taarifa ilimfikiaje Makonda hadi amemtuma afikiaje hadi kumtuma yeye afike Mahakamani kumuwakilisha kwenye shauri hilo.

Wakili Reginald amejibu hoja hiyo akidai kuwa mteja wake alipata taarifa hizo kupitia vyombo vya habari hivyo akaona afike Mahakamani hapo licha ya kwamba mteja wake hakupewa samansi.

Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Subira Mwalumuli, ameeleza mahakama hiyo kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini DPP wanakusidia kupeleka mapingamizi ya awali dhidi ya maombi yaliyowasilishwa kwenye kesi hiyo kwa madai kuwa ufunguaji kesi hiyo una mapungufu ya kisheria.

Hakimu Lyamuya ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 25 mwaka huu, ambapo wajibu maombi watatakiwa kuwasilisha hati kinzani huku upande wa Jamhuri (DCI na DPP) wakiwatakiwa kuwasilisha hoja za mapingamizi yao juu ya shauri hilo.