Dawa za kulevya kilo 250 zateketezwa Mtwara

0
309

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imeteketeza kilo 250.7 za dawa za kulevya zinazojumuisha kilo 51.7 za heroin na kilo 199 zenye mchanganyiko wa Heroin na Cocaine

Kamishna wa DCEA, Gerald Kusaya amesema utekelezaji huo ni amri ya mahakama iliyotolewa katika kesi namba 2 ya mwaka 2018 kwenye kikao cha mahakama kuu kilichoketi Novemba 2021 mkoani Lindi mbele ya jaji Latifa Mansour.

Kesi hiyo iliwahusisha washtakiwa Sano Sidiki na Tukure Ally ambao wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja.

Amri nyingine ya utekelezaji ilitolewa na Jaji Isaya Arufan Novemba 2021 kwenye kesi nba 25 ya mwaka 2019 iliyowahusisha washitakiwa Mohamed Nyamvi na Ahmad Said Mohamed.

Katika kesi hiyo washitakiwa hao wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja.

Zoezi hilo limefanyika kwa mujibu wa kanuni namba 14 ya kanuni za kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya namba 5 ya mwaka 2015.

Kamishna huyo amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vinavyojihusisha na mapambano dhidi ya dawa za kulevya.