Makamu wa Rais msibani kwa Malecela

0
181

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango akiongozana na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango leo wamefika nyumbani kwa Waziri Mkuu Mstaafu John Malecela Kilimani Jijini Dodoma kutoa pole kufuatia kifo cha mtoto wake Dkt. Mwele Ntuli Malecela kilichotokea tarehe 10 Februari 2022 Geneva Nchini Uswisi.

Akitoa neno la faraja kwa familia na waombolezaji mbalimbali waliojitokeza nyumbani hapo, Makamu wa Rais amewasihi kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu pamoja na kumuombea marehemu apate pumziko la Amani.

Makamu wa Rais amemtaja Dkt. Mwele kama shujaa aliejitoa kupigania Afya za wananchi wengine kupitia tafiti mbalimbali alizokuwa akizifanya zenye lengo la kusaidia jamii kupambana na magonjwa mbalimbali.

Amesema Dkt. Mwele alifanya kazi iliyo njema na kuonekana katika jamii ndani na nje ya nchi.

Aidha Makamu wa Rais amesema katika kipindi cha uhai wake Dkt. Mwele Malecela aliinua jina la Tanzania kwa kuaminiwa kufanya kazi katika taasisi kubwa ya afya duniani.

Amesema uwezo wa Dkt. Mwele katika kazi pia uliinua wanawake hapa nchini hivyo hakuna budi kumshukuru Mungu kwa zawadi hiyo pamoja kumuombea ampokee ili apumzike kwa Amani.