Mbowe na wenzake wana kesi ya kujibu

0
307

Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu imemkuta na kesi ya kujibu, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu katika mashitaka 5 kati ya 6 hivyo wanapaswa kuanza kujitetea.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Joachim Tiganga ambapo amesema mahakama imepitia ushahidi wote wa Jamhuri wa Mashahidi 13 ambao umewafanya Washitakiwa wakutwe na kesi ya kujibu.

Hata hivyo Mahakama hiyo haijamkuta na kesi ya kujibu mshtakiwa wa kwanza katika shitaka la sita la kukutwa na sare na vifaa vya Jeshi licha ya kwamba atajitetea katika makosa mengine.

Kufuatia uamuzi huo, Mahakama hiyo itaanza kusikiliza ushahidi wa upande utetezi ukiongozwa na wakili Peter Kibatala ambao wamesema watakuwa na mashahidi zaidi ishirini ifikapo Machi 3,2022.