January: Tupeni muda

0
176

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema serikali inaendelea kuchukua hatua kadhaa kuhakikisha bei za mafuta hazipandi pamoja na umeme kupatikana kwa uhakika kwani wanatambua ni nyenzo muhimu katika ustawi wa uchumi.

Waziri Makamba amesema hayo wakati akitolea ufafanuzi baadhi ya masuala yaliyoibuliwa na kamati ya bunge hasa kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Amesema kukatika huko kwa umeme kunasababishwa na mambo kadhaa ikiwemo uchakavu wa miundombinu pamoja na vifaa ambavyo vinatumika kusambaza nishati hiyo.

Amesema mtangulizi wake, Dkt. Medard Kalemani amekaa wizarani hapo kwa miaka minne, huku Rais Dkt. Magufuli amekaa madarakani miaka sita, lakini yeye ana miezi minne na Rais Samia Suluhu ana mwaka mmoja, hivyo ameomba wapewe muda, ili wapimwe kwa matokeo.

Kuhusu ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), amesema mkandarasi sasa anasimamiwa kwa karibu zaidi kuliko ilivyokuwa na lengo ni kuhakikisha mradi unakamilika salama na kuwanufaisha wananchi.

Aidha, amesema karibuni watasaini hati ya makubaliano ya kuboresha mfumo wa kupokea mafuta bandarini ambapo mfumo mpya utakuwa na uwezo wa kupokea mafuta mara tatu zaidi ya mfumo wa sasa, ili kupunguza muda ambao meli zinasubiri kupakua mafuta bandarini.