Mchengerwa – Tanzania kucheza kombe la Dunia

0
165

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mohamed Mchengerwa amesema Tanzania inatarajia kushiriki kwenye mashindano ya kombe la dunia baada ya kumalizika mashindano ya mwaka huu 2022 yatakayofanyika Qatar kutokana na mikakati kabambe ya maandalizi inayoendelea hivi sasa.

Waziri Mchengerwa ameyasema haya leo Februari 8, 2022 jijini Dar es Salaam kwenye halfa iliyoandaliwa na ubalozi wa Qatar, kuadhimisha siku ya michezo ya nchi hiyo inayofanyika kila Jumanne ya mwezi Februari kila mwaka, ambapo Balozi Hussain bin Ahmad Al Homaid na Waziri Mchengerwa waliongoza mazoezi ya kutembea uwanjani kama ishara ya ushiriki wa maadhimisho ya siku hiyo.

Katika halfa hiyo aliambatana na Katibu Mkuu wake, Dkt. Hassan Abbasi, Naibu Katibu Mkuu, Saidi Yakubu na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha, Amesema Tanzania inakusudia kushiriki katika mashindano hayo kutokana na mikakati kabambe iliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya michezo nchi nzima.

“Sisi kama taifa ni muhimu tukubali ili kufanikisha zoezi hili la kushiriki mashindano makubwa kama haya lazima kujiandaa na kuboresha miundombinu ya michezo ambapo kwa sasa tumeshatenga shule 56 nchi nzima kwa ajili ya michezo”. Amefafanua Mchengerwa.

Aidha, amesema Serikali inakusudia kujenga viwanja vikubwa vya ndani ambavyo vinajumuisha michezo mbalimbali viwili kwenye mkoa wa Dar es Salaam na kimoja Dodoma

Amemwomba Balozi wa Qatar Hussain Bin Ahmad Al Homaid kuiomba Serikali ya nchi yake kuisaidia Tanzania kwenye eneo la miundombinu ili kuendelea kuimarisha uhusiano uliojengeka baina ya nchi hizo mbili.

Amemhakikishia Balozi kuwa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ipo tayari kuendelea kushikiana wakati wowote kwenye sekta za michezo, Sanaa na Utamaduni kwa faida ya wananchi wa nchi zote mbili.

Kwa upande wake Balozi Al Homaid ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwa na uhusiano mzuri na nchi yake na kubainisha kuwa nchi yake imetenga siku ya michezo ili kuendeleza michezo na kuwafanya wananchi wake kuepukana na magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa kufanya mazoezi.

Amesema kuwa nchi yake inakwenda kuwa nchi ya kwanza miongoni mwa nchi za kiarabu kuwa mwenyeji wa mashindano ya kombe la dunia.

Katika Hafla hiyo Mchengerwa na Balozi Al Homaid walipiga mpira wa miguu golini kuashiria ufunguzi rasmi wa siku hiyo huku timu ya ubalozi huo na ile ya watumishi wa shirika la ndege la nchi hiyo wakicheza mechi ya kirafiki na timu ya ubalozi na kufungwa mabao 8-2 dhidi ya timu ya Shirika la ndege la Qatar.