Serikali ya Mkoa wa Mara imemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa miradi ya maendeelo iliyoletwa mkoani humo ikiwemo miradi ya Afya, elimu, barabara na maji.
Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa miundombinu ya kusafisha na kutibu maji katika mradi wa maji ya Nyabehu, Mkuu wa Mkoa huo Ally Hapi amesema Mkoa wa Mara unashukuru kwa hatua hiyo ambayo inakwenda kuchochea maendeleo.
Hapi amesema kwa upande wa Elimu wameweza kujenga madarasa 708 ambapo katika madarasa hayo wameweza kujenga Ofisi za Walimu 219.
Amesema kujengwa kwa madarasa hayo kumewezesha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo kupata fursa ya kuanza masomo kwa awamu moja.
Akigusia miradi ya maji Hapi amesema, kwasasa mkoa wa Mara una miradi mingi ya maji ambayo tayari imeshaaanza kutumika, huku miradi mingine ikiendelea chini ya Ruwasa pamoja na mamlaka nyingine.
Amesema awali mkoa wa Mara ulikuwa ukipata maji ambayo si safi na salama, lakini kwa sasa wananchi wanapata maji safi na salama huku miradi mingine ikiendelea kuanzishwa ili kupambana na hali hiyo.
Kuhusu miundombinu ya barabara Hapi amesema miundombinu hiyo inaendelea kuboreshwa huku kukiwa na barabara kadhaa zilizo katika hatua ya mwisho kumalizika.
Kwa upande wa Afya Hapi amesema, Serikali ya awamu ya sita imeleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya katika halmashauri mbalimbali mkoani.
Hapi amemuhakikishia Rais usimamizi bora wa miradi hiyo huku akiongeza kuwa hayuko tayari kuona watumishi wasio waaminifu wakiharibu wakiharibu au kuchelewesha miradi.