Wanaume watwishwa jukumu la kukomesha ukeketaji

0
190

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wanaume kujitokeza kupiga vita vitendo vya ukeketaji, kwani baadhi ya wanawake hukeketwa au wazazi hukeketa watoto wao wakiamini kwamba ndio wenye nafasi kubwa ya kuolewa.

Dkt. Gwajima ametoa wito huo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukeketaji kwa wanawake na watoto, ambayo huadhimishwa Februari 6 ya kila mwaka.

Amesema licha ya jitihada za serikali kuwezesha kupunguza tatizo hilo ambalo ni sehemu ya ukiukwaji wa haki za binadamu, Waziri Gwajima amesema bado baadhi ya makabila yanafanya vitendo hivyo kwa sababu za kimila, umaskini au kama njia ya kumwingiza mtoto wa kike kwenye umri wa usichana.

Ameitaja mikoa inayoongoza kwa ukeketaji Tanzania kuwa ni Manyara (58%), Dodoma (47%), Arusha (41%), Mara (32%) na Singida (31%).

Dkt. Gwajima amesema, kwa mujibu wa utafiti uliofanyika, mwanamke mmoja kati ya 10 mwenye umri wa miaka 15 hadi 45 amekeketwa, ambapo 30% kati yao walikeketwe kabla ya kufikisha umri wa mwaka mmoja.

Maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika kitaifa mkoani Mara huku mikoa mingine yenye maambukizi makubwa zikiadhimisha kwenye ngazi ya mkoa.