Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amesema kuwa mgao mkubwa wa umeme ambao ulikuwa ukitarajiwa hautakuwepo, kutokana na TANESCO kupata njia mbadala za kuupunguza.
Amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina aliyetaka kujua sababu hasa ya kukatika kwa umeme nchini na Wizara inafanya nini kuwanusuru Watanzania.
Akijibu, amesema kwamba mgao mkubwa na mkali hautakuwepo baada ya wizara kufanyia kazi maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Ametaja mambo yaliyopunguza ukali wa mgao wa umeme kuwa ni;
- Wamebaini kwamba wanaweza kupitisha kiasi cha gesi kwenye mitambo ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), na hivyo kufidia upungufu wa gesi ambayo ungetokea kutokana na matangenezo ya mitambo ya PAET.
- Kwa sasa mabwawa ya kufua umeme yameanza kurudi katika hali nzuri na hivyo yataweza kuongeza kiwango cha uzalishaji na kusaidia maeneo ambayo yalikuwa yakose umeme.
- Walitarajia kwamba kungekuwa na uhitaji mkubwa sana wa umeme, lakini baada ya kufanya uchunguzi wamebaini kwamba kile walichodhani kitahitajika, sicho kinachohitajika. Ameeleza kwamba awali walidhani watahitaji takribani megawati 300, lakini uhalisia unaohitajika ni megawati 100
“Nitoe kauli ya serikali kwamba, ule mgao tuliokuwa tunautarajia utakuwepo kwa makali yale na ukubwa ule, hautakuwepo,” amesema Byabato akiongeza kwamba watahakikisha Watanzania wanaendelea kupata umeme.
Amesema katika kipindi cha mgao mdogo wa umeme, watatumia nafasi hiyo kufanya marekebisho ikiwemo kupunguza umeme kwenye njia zilizozidiwa, kukata miti ambayo imekuwa ikiangukia nguzo, na kuboresha vituo vya kupoza umeme.