Dkt. Mpango: Mabalozi tambueni vipaumbele vya taifa

0
220

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewaasa Mabalozi kutambua vipaumbele vya taifa ikiwa ni pamoja na kufahamu takwimu za msingi ikiwemo Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025, Dira ya taifa na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano zitakazochagiza katika kutafuta wawekezaji.

Dkt. Mpango ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali,mazungumzo yaliofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Mabalozi hao ni wale wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kuwait, Israel ,Brazil na Urusi, pia Makamu wa Rais amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa na kusema imani waliopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuliwakilisha taifa kwenye nchi hizo ni kubwa.

Aidha amesema ni muhimu kwa Mabalozi hao kufanya jitihada za makusudi kuzifahamu vema nchi wanazokwenda kuiwakilisha Tanzania ili kuweza kujifunza misingi ya ukuzaji wa uchumi wao na kuhamisha maarifa hayo kwa taifa la Tanzania.

Amesema katika kutekeleza diplomasia ya uchumi Mabalozi hao wanapaswa kuongeza ushirikiano na vongozi wa sekta binafsi ili kuwavutia kuwekeza Tanzania wakizingatia kwenda kufanya kazi kwa weledi na uzalendo kwa maslahi ya taifa.

Amesema ni muhimu kwa Mabalozi hao kuendeleza na kukuza ushirikiano baina ya Tanzania na nchi wanazokwenda kuliwakilisha taifa na kuitangaza lugha ya Kiswahili katika nchi hizo ikiwemo kutafuta fursa ya kufundishwa kwa lugha hiyo katika nchi wanazokwenda kuiwakilisha

Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika kutekeleza diplomasia ya uchumi hivyo amewataka Mabalozi hao kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi utakaokuwa na manufaa kwa Tanzania

Pia amewaagiza Mabalozi hao Kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini pamoja na kutafuta fursa za ushirikiano hasa katika taasisi za utalii, utafiti na maendeleo.

Makamu wa Rais amesema Tanzania imeweka msisitizo katika kuleta mabadilizo katika uwekezaji pamoja na kuimarisha sekta ya viwanda hivyo amewasihi mabalozi hao kujielekeza katika kutafuta teknolojia rafiki zitakazosaidia katika kukuza na kuendeleza viwanda kulingana na mazingira ya hapa nchini.