Majaji watakikwa kuzijua sheria za Afrika Mashariki

0
151

Rais wa mahakama ya Jumuiya Afrika Mashariki Nesto Kayobera amesema mafunzo yanayohusu sheria za jumuiya hiyo ni muhimu kutolewa kwa Majaji wa nchi wanachama ili kuwajengea uwezo wa kutoa maamuzi ya haki kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.

Jaji Kayobera ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam mara baada ya mafunzo ya siku mbili yaliyotolewa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu hapa nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo juu ya sheria mbalimbali zinazohusisha nchi za Afrika Mashariki.

Aidha Jaji Kayobera amebainisha kuwa Mahakama ya Afrika Mashariki kwa sasa imetimiza miaka ishirini tangu kuanzishwa kwake lakini bado kuna baadhi ya Majaji hawajui sheria zake hivyo ni vyema kubadilishana mawazo ili kutatua changamoto zinazokabili wananchi Jumuiya hiyo.

“Ni aibu kubwa sana kuona Majaji wengi hawajui sheria za Jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo mafunzo haya yatawajengea uwezo Majaji hawa kupata uzoefu katika kuendesha kesi kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki”Amesema Jaji Kayobera.

Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo Girama Francis kutoka ALP East Africa Group amesema hatua hiyo ya kutoa mafunzo kwa Majaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki utaleta muunganiko mzuri kwa Majaji kushirikishana changamoto zinazohusiana na utoaji wa haki.