TCRA imekifungia kipindi cha Efatha Ministry

0
285

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA imekifungia kwa miezi mitatu kipindi Cha Efata Ministry Cha Askofu Josephat Mwingira kinachorushwa na Star TV kwa kurusha maudhui yenye ukakasi kwenye jamii Desemba mwaka 2021.

Pia kituo hicho kimepewa onyo kali na kutakiwa kuomba radhi kwa siku tatu kuanzia Januari 25 mwaka huu kwa wasikilizaji wake na Watanzania kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Habbi Gunze amesema uamuzi huo umekuja baada ya kamati ya maudhui kupitia kipindi hicho na kubaini kukiukwa kwa kanuni na sheria za utangazaji wa radio na televisheni.

Gunze ameeleza kuwa kamati pia imebaini kuwa kipindi kilitoa taarifa za upotoshaji na zisisizo na uthibitisho wowote kuhusu uchaguzi na utendaji wa viongozi wa Serikali, hali inayosababisha chuki baina ya Watanzania kwa viongozi wao.

Amesema Askofu Mwingira katika mahubiri yake alidai, “Mwaka jana nikamwambia Mungu, Polisi wenyewe waligawanyika makundi mawili, jeshi makundi mawili, yaani wangechapana vizuri.”

Maudhui hayo yameelezwa kukiuka kanuni za maudhui ya utangazaji yanayoweza kuleta chuki, uchochezi na taharuki miongoni mwa jamii.

Pia imeelezwa Star TV wameonesha udhaifu katika kusimamia kipindi hicho kinachorushwa kwa matangazo ya Moja kwa moja hivyo kuruhusu maudhui yenye ukakasi kama ambavyo wamekiri wenyewe kinyume na kanuni ya 37 (1) (a) ya kanuni za mawasiliano ya kielekroniki na posta ya Utangazaji wa redio na Televisheni ya Mwaka 2018.

Kutokana na kosa hilo Star TV na vyombo vingine vya Habari vimetakiwa kuhakikisha vinazingatia sheria na kanuni za maudhui za radio na Televisheni ili kuepusha hali ya sintofahamu kwenye jamii.

Hata hivyo baada ya kutolewa kwa adhabu hiyo Star TV imepewa nafasi ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwenye Baraza la ushindani wa haki kibiashara ndani ya siku 21 kuanzia siku ya kutolewa kwa uamuzi huo.