Inspecta wa Polisi Innocent Ndowo kutoka kitengo Cha Uchunguzi wa Kisayansi juu ya Makosa ya kimtandao, katika kesi ya Uhujumu Uchumi yenye mashtaka ya Ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA freeman Mbowe na wenzake watatu amekabidhi Mahakama simu nane za mkononi alizozifanyia uchunguzi ziwe sehemu ya ushahidi wake Mahakamani.
Shahidi huyo wa 10 katika mashahidi 24 wanaotakiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo kwa upande wa jamhuri amekabidhi vielelezo hivyo baada ya kuhojiwa na wakili wa Serikali Mwandamizi Pius Hilla juu ya uchunguzi alioufanya kwenye vielelezo hivyo.
Katika maelezo yake shahidi huyo amedai kwamba amefanya uchunguzi wa vielelezo hivyo baada ya kupewa jukumu hilo na Ofisi ya DCI ili kubaini mawasiliano pamoja na miamala ya fedha yaliyofanyika kwenye namba ya simu za Mbowe, Halfan Bwire na Denis Urio kati Juni Mosi hadi Julai 31 mwaka 2020.
Amedai vifaa hivyo alivyovipokea ikiwemo simu za Tekno,Itel na Sumsung na laini za simu Agost 13 mwaka 2020 kisha akavihifadhi kwenye loka lake hadi Julai Mosi mwaka 2021 alipoanza kuvifanyia uchunguzi baada ya kutakiwa kufanya hivyo na wapelelezi.
Kwa Upande wa Utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala shahidi huyo amehojiwa na wakili Nashaon Nkungu na John Malya ambao walitaka kujua iwapo shahidi huyo katika uchunguzi wake alibaini taarifa yoyote inayohusiana na vitendo vya kigaidi kwa mshtakiwa Hassan Bwire, Adam Kasekwa na Freeman Mbowe.
Akijibu hoja hiyo shahidi huyo amedai hajui chochote kuhusiana na mashataka ya washitakiwa hao kwa sababu kazi aliyokuwa amepewa ni kuchunguza mawasiliano ya namba za simu na miamala ya fedha kwenye namba husika pamoja na usajili wa namba hizo zilizoainishwa kwenye barua iliyotoka ofisi ya DCI
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 19,2021 ambapo Upande wa Utetezi utaendelea kumuhoji shahidi huyo.