Mahakimu 29 wala kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania

0
172

Kuongezeka kwa mahakimu 29 katika Mahakama za Mwanzo nchini kutaharakisha usikilizwaji wa kesi na kufanya maamuzi ya hukumu  kwa haraka kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma wakati akiwaapisha mahakimu wateule 29 ambao wanakwenda kufanya Kazi Katika Mahakama za Mwanzo mbalimbali hapa nchini.

Profesa Juma amewataka wateule hao kwenda kufanya kazi kwa uadilifu kwenye vituo vyao vya kazi na kuongeza juhudi ya kusoma ili kuendana na ulimwengu wa sasa na mazingira yake.

“Nikiangalia sura zenu, ninyi ni vijana sana naona sura zitakazofanya kazi miaka 25 ijayo. Leo ni hatua ya kwanza ya safari na jamii itawapa heshima maana mnavishwa vazi la uheshimiwa. Zama zimebadilika sana, mtagundua elimu ya sheria mliyopata shuleni mtakutana na changamoto katika utendaji kazi wenu, hivyo mnapaswa kusoma sana kazi za mahakama na kujua mikataba ya kazi zako zinasemaje,” amesema Prof. Juma

Aidha, ameongeza kuwa mahakimu hao wajiepushe na kusikiliza maelekezo ya watu wengine wakiwa wanaamua kesi, badala yake watende haki kwa pande zote mbili.