Serikali yaipa DAWASA kazi mpya

0
162

Wizara ya Maji imetangaza kuongeza eneo la huduma kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), ili kusogeza huduma ya maji kwenye kijiji cha Kisaki na Kikwete kilichopo Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani.

Uamuzi huo umekuja mara baada ya Mbunge wa Kisarawe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano – Mazingira na Dkt. Selemani Jafo kutoa ombi kwa Wizara kuipa DAWASA jukumu la kupeleka maji kwenye kijiji cha Kisaki na Kikwete baada ya RUWASA kushindwa kutekeleza kutokana na ufinyu wa bajeti.

Akitangaza uamuzi huo wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa maji Kibamba – Kisarawe, Waziri wa Maji Jumaa Aweso, amewataka DAWASA kufikisha huduma ya maji kwenye eneo hilo kutoka kwenye mradi wa Kibamba – Kisarawe.

Waziri Jafo ameipongeza DAWASA kwa kazi kubwa ya kutekeleza mradi wa maji Kibamba – Kisarawe kwa bilioni 10.6 kwa Wilaya ya Kisarawe, hii imesaidia sana kuimarisha upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Kisarawe.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja ameeleza kupokea jukumu hilo na kusema kazi ya kufikisha maji Kisaki – Kikwete itatekelezwa ndani ya miezi mitatu kutoka sasa.

Mradi wa maji Kibamba – Kisarawe unazalisha lita milioni 6 za maji kwa siku ambayo ni zaidi ya mahitaji ya maji kwa Wilaya ya Kisarawe ambayo ni lita milioni 1.