Baada ya miaka 14, Zuhura Yunus aiaga BBC

0
401

Mtangazaji mashuhuri wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Zuhura Yunus leo usiku atatangaza kwa mara ya mwisho kipindi chake cha mwisho katika shirika hilo.

Tangu mwaka 2008 baada ya kujiunga na BBC, Zuhura amekuwa akitangaza vipindi mbalimbali vya TV na redio pamoja na kuandaa vipindi mbalimbali vya redio na televisheni.

Zuhura alikuwa mtangazaji wa kwanza mwanamke kutangaza Dira ya Dunia na mwanamke wa kwanza kutoka Tanzania kutangaza kipindi cha Focus on Africa TV na mtu wa kwanza kutangaza BBC World News akiwa amevaa hijabu.

Miezi michache iliyopita alizindua kitabu alichoandika kuhusiana na wasifu wa Biubwa Amour Zahor, Mwanaharakati wa kisiasa mwanamke wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar.

Wakati wa utendaji wake BBC amewahi kuwahoji watu mashuhuri ikiwemo Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, pamoja na Edward Lowassa alipokuwa mgombea urais wa upinzani mwaka 2015.

Zuhura aliwahi kufanya makala ya kipekee ihusuyo meli ijulikanayo kama MV Liemba iliyojengwa na Wajerumani wakati wa vita ya kwanza ya dunia na bado inatumika hadi sasa huko Kigoma.