Walioapishwa waagizwa kushughulikia kero za Wananchi

0
203

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Viongozi mbalimbali walioteuliwa hivi karibuni na kuapishwa hii leo na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa karibu na Wananchi na kusikiliza kero zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi.

Akizungumza Ikulu Chamwino mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha Viongozi mbalimbali walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema kuwa matarajio ya Rais ni kuona Viongozi hao wanatatua kero mbalimbali zinazowakabili Wananchi.

Amewataka kufanya kazi kwa weledi na kuheshimu mamlaka zao za uteuzi pamoja na kuwaheshimu wale wanaowatumikia.

Viongozi walioapishwa hii leo na Rais Samia Suluhu Hassan ni pamoja na Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu,

Mawaziri walioapishwa ni pamoja na Nape Nnauye anayekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Hamad Masauni anayekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt, Pindi Chana ameapishwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Hussein Bashe anakuwa Waziri wa Kilimo na Dkt. Angelina Mabula ameapishwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Wengine walioapishwa hii leo na Rais Samia Suluhu Hassan ni Antony Mavunde kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Jumanne Sagini kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Lemomo Ole Kiruswa ameapishwa kuwa Naibu Waziri wa Madini, Atupele Mwakibete kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi anayeshughulikia sekta ya Uchukuzi na Ridhiwan Kikwete ameapishwa kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.