Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa mkuu wa mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti kufuatia vifo vya watu 14 waliofariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea katika kijiji cha Lidumbe wilaya ya Newala mkoani Mtwara.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mtwara, Mark Njera amesema chanzo cha ajali hiyo iliyotokea katika barabara ya Uchumi, Mtwara – Tandahimba -Newala – Masasi ni mwendokasi wa dereva wa gari aina ya Scania ambaye alishindwa kulimudu na kwenda kuwagonga watu hao na kusababisha vifo hivyo pamoja na majeruhi wengine 22.
Rais Samia Suluhu Hassan amemtaka mkuu wa mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Gaguti kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa wote, ndugu, jamaa, marafiki na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Pia amewaombea kwa Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema peponi, Amina.
Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan amevitaka vyombo vyote vinavyosimamia usalama wa barabarani kuongeza juhudi za kudhibiti ajali hasa katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka, na pia amewaasa madereva kufuata na kuzingatia Sheria za usalama barabarani.