Waziri Mbarawa aridhishwa na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma

0
181

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema kukamilika kwa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma uliopo Mkoani Mara utafungua fursa zaidi katika mikoa ya kanda ya ziwa.

Profesa Mbarawa ameyasema hayo wakati akikagua ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilometa 1.75 ambapo utaruhusu ndege za aina mbalimbali kutua kwa urahisi kiwanjani hapo.

Profesa Mbarawa amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 35.047 na mkandarasi anayetelekeza mradi huo ni Beijing Construction Company Limited ambapo kazi zinaendelea kwa kasi.

“Kiwanja cha Ndege cha Musoma kitakapokamilika kitafungua anga kwa kiasi kikubwa na kukuza uchumi wa mkoa wa Mara na mikoa jirani”, amesema Profesa Mbarawa.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma, Frank Msoffe amesema kuwa ujenzi wa kiwanja hicho utakapokamilika utatoka katika daraja la 2C na kwenda 3C na kuruhusu kupokea ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 70 hadi 80.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mara Mhandisi Vedastus Maribe, ameeleza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2022 na unahusisha barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya maegesho ya ndege, jengo la kuongezea ndege na jengo la zima moto.