Ndejembi ataka maboresho mradi wa nyumba Gezaulole

0
151

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Deogratius Ndejembi ameuagiza uongozi wa Kampuni ya Nyumba za Watumishi ambayo ndio mmiliki wa nyumba ambazo watumishi wa umma wamepanga, kuhakikisha hadi kufikia Januari 28 mwaka 2022 uwe umekamilisha ujenzi wa uzio kwenye mradi wa nyumba uliopo Gezaulole, Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Naibu Waziri Ndejembi ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo na kuzungumza na wapangaji ambao ni watumishi wa umma, ambapo pia ametatua changamoto zilizokua zikiwakabili wapangaji hao.

Amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwenye ujenzi wa mradi huo ili kutoa huduma ya makazi kwa Watumishi wake, hivyo ni lazima kampuni hiyo ya Nyumba za Watumishi ikahakikisha inamaliza changamoto zote zilizobaki katika mradi huo wa nyumba uliopo Gezaulole.

” Nimekuja hapa baada ya kusikia malalamiko kutoka kwa wapangaji wa nyumba hizi ambao ni Watumishi wetu wa umma, niuagize uongozi wa Watumishi Housing kuhakikisha changamoto zote ambazo wapangaji wamezisema ikiwemo ya kizima moto, ujenzi wa ukuta na kuongeza walinzi zinatatuliwa hadi kufikia Januari 28, 2022.” ameagiza Naibu Ndejembi

Kuhusu changamoto ya kiusalama kwenye makazi hayo, Naibu Waziri Ndejembi ameuagiza uongozi wa kampuni hiyo kuhakikisha hadi kufikia Januari Mosi mwaka 2022 unaongeza idadi ya walinzi wanaolinda eneo hilo ili kuleta uhakika wa usalama wa watu na mali.