Koffi Olomidé afutiwa mashtaka ya udhalilishaji

0
2560

Mahakama ya rufani nchini Ufaransa imetengua hukumu ya kesi iliyokuwa ikimkabili mwanamuziki wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Antoine Agbepa Mumba, maarufu Koffi Olomidé ambaye alitiwa hatiani kwa kosa la kuwadhalilisha kingono wanenguaji wake wanne wa zamani, lakini ametiwa hatiani kwa mashtaka mengine.

Mahakama hiyo imetengua hukumu iliyotolewa miaka miwili iliyopita ambapo alitiwa hatiani kwa kumdhalilisha mmoja wa waliokuwa wanenguaji wake akiwa na umri wa miaka 15.

Ilielezwa kwamba alitenda kosa hilo mjini Paris, Ufaransa kati ya mwaka 2002 na 2006.

Hata hivyo nguli huyo wa miondoko ya rumba na soukous alipewa adhabu ya kifungo cha nje na kutakiwa kutotenda kosa kwa muda wa miezi 18.

Pia aliamriwa kuwalipa wanenguaji hao fidia ya kati ya shilingi milioni 25 na shilingi milioni 83 za Kitanzania.