Rais Samia awaonya polisi wanaotumia nguvu kukamata watuhumiwa

0
227

Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Polisi kufuata sheria katika utendaji kazi wake na kumaliza kero zinazolalamikiwa na wananchi.

Akitaja baadhi ya mambo yanayolalamiliwa, Rais amesema ni pamoja na kutumia lugha isiyofaa katika kazi zao, kukamata watu kwa kutumia nguvu na kukamata watu kwa makosa yasiyo ya msingi ambayo wakati mwingine wanahitaji kuelimishwa tu.

Rais Samia amesema vitendo vya rushwa na askari kujiona kuwa na nguvu isiyohojiwa kwa wananchi huliondolea Jeshi hilo uaminifu kwa wananchi wanyonge.

Amesema hayo wakati Mafunzo ya Uofisa Kozi Na. 01/2020/2021 (Warakibu Wasaidizi wa Polisi – ASP) ambapo amewataka wahitimu kutumia mafunzo hayo kuwatumikia wananchi na kuboresha taswira ya polisi.

Akitoa taarifa ya mafunzo hayo yaliyoanza Juni 18, 2021, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ambaye ndiye mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini, jijini Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema maofisa 747 wamehitimu ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa chuo mwaka 1961.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea maofisa wa polisi uwezo na kuimarisha viwango vya weledi katika utendaji kazi wao.

Miongoni mwa mafunzo yaliyotolewa ni kozi za kwata na gwaride, misimamo mikali na ugaidi, uongozi wa polisi, upelelezi wa makosa ya kigaidi, matumizi ya silaha na mbinu za kujihami.

Serikali imepandisha vyeo maafisa, wakaguzi na askari polisi, kuajiri askari mbadala na askari wapya wapatao 4,103, kuipandisha hadhi Hospitali ya Polisi iliyopo barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.