Vikwazo 46 kati ya 64 vya kibiashara vilivyokuwa vikikwamisha biashara kati ya Tanzania na Kenya vimeondolewa, na majadiliano yanaendelea ili kumaliza vikwazo vyote.
Kauli hiyo imetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa mkutano na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam akiwa na mgeni wake Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya baada ya viongozi hao kumaliza mazungumzo yao ya faragha.
Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza kuwa kuondolewa kwa vikazo hivyo ni matunda ya ziara yake aliyoifanya nchini Kenya.
Aidha amesema wamekubaliana kufanya biashara ya gesi kutoka Tanzania kwenda Kenya na kwamba wamewaelekeza Mawaziri na Watendaji wengine kuendelea kukamilisha taratibu za mradi wa kuunga mabomba ya kusafirisha gesi hiyo kutoka Tanzania kwenda Kenya.
“Tumekubaliana kufanya biashara ya kuwauzia gesi kutoka Tanzania, hivyo mawaziri na watendaji wengine wataendelea kukamilisha taratibu za mradi wa kuunga mabomba ya kusafirisha gesi kutoka Tanzania kwenda Kenya.” Rais Samia Suluhu Hassan
Naye Rais wa Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema kuwa kupungua kwa vikwazo vya kibiashara kati ya Tanzania na Kenya kumeimarisha ushirikiano katika sekta ya biashara pamoja na masuala ya kidiplomasia.
Ameongeza kuwa, kukamilika kwa mradi wa kusafirisha gesi kutoka Tanzania kwenda Kenya kutasaidia Wananchi wa Afrika Mashariki kujiimarisha zaidi kiuchumi.
“Hakuna haja kununua mafuta kutoka kwa nchi za mbali wakati ndugu zetu Watanzania wamebarikiwa kupata gesi ambayo itasaidia kupata maendeleo, na itasaidia Wananchi wa Afrika Mashariki.” amesema Rais Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta amekamilisha ziara yake ya siku mbili nchini na tayari ameondoka nchini.