Dkt. Mpango asisitiza suala la usawa Afrika

0
172

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amesema ili kufikia ajenda ya Afrika Tuitakayo, Bara la Afrika linahitaji usawa katika uongozi, uwakilishi sawa katika masuala ya siasa pamoja na mazingira ya usawa katika masuala ya kijamii na kiuchumi.

Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha awali cha nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika cha jukwaa la kujadili masuala ya usawa wa kijinsia, kikao kilichofanyika kwa njia ya mtandao.

Amesema kwa upande wa Tanzania, Serikali inatambua kuwa usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji Wanawake kiuchumi ni nguzo muhimu katika kufikia maendeleo endelevu kwa jamii yeyote ile, ndio maana imekua ikiingia katika mikataba ya kitaifa, kikanda na kimataifa inayohusu kuimarisha usawa wa kijinsia, kuwawezesha Wanawake kiuchumi pamoja na kuimarisha uwezo wa Wanawake katika uongozi na nafasi za maamuzi katika sekta zote za maendeleo.

Amesema mchango wa Wanawake katika ukombozi wa Bara la Afrika na hata baada ya kupata Uhuru ni mkubwa bila kujali uwepo wao mstari wa mbele au mchango wao kwa waliopo mstari wa mbele.

Hata hivyo Makamu wa Rais amesema pamoja na kuongezeka kwa idadi ya Wanawake katika ufanyaji biashara na kazi, bado Bara la Afrika lina idadi ndogo ya uwakilishi wa Wanawake katika vyombo vya maamuzi.

Dkt. Mpango amesisitiza kuwa, Tanzania inaendelea kutekeleza ahadi zake ilizotoa katika Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa ambazo zililenga kukuza na kulinda haki za kiuchumi kwa Wanawake.

Kikao hicho cha awali cha nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika cha jukwaa la kujadili masuala ya usawa wa kijinsia kinachagizwa na kauli mbiu isemayo kuimarisha upatikanaji wa fursa kwa Wanawake katika uongozi na nafasi za maamuzi ili kufikia ajenda ya Afrika tunayoitaka, na ni maandalizi ya mkutano mkuu wa Viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari mwaka 2022.