Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu amesema, Serikali imetoa mwongozo mpya kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatoa mikopo kwa watu wenye ulemavu bila sharti la kuungana ama kikundi.
Mwongozo huo unatoa ruhusa kwa watu wenye ulemavu kupatiwa mikopo hiyo bila sharti la kuwa na kikundi ama kuungana kama ilivyokuwa hapo awali na kwamba hata mtu mmoja mmoja anaweza kupata mkopo kutoka katika halmashauri yake.
“Naomba kutumia hadhara hii kutoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuanza kutumia mwongozo mpya ambao unaelekeza kuwa mtu mwenye ulemavu anaweza kupatiwa mkopo bila ya kuwa katika kikundi.” amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema lengo la mwongozo huo ni kuwawezesha watu wenye ulemavu kupata mikopo bila masharti magumu, na hivyo kupiga hatua za kimaendeleo kwa haraka.
Awali akimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Tanga, Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema, azma ya Serikali ni kuona watu wenye ulemavu wanashirikishwa katika mambo yote muhimu ya ujenzi wa Taifa.
Waziri Mhagama amesema, hivi sasa Serikali imeweka mazingira wezeshe kwa watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuingia katika nafasi za maamuzi Serikalini.
Maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani hufanyika kila ifikapo Desemba 3 ambapo hapa nchini watu wenye ulemavu wamekutana kwa siku 3 mkoani Tanga kujadili mambo mbalimbali yanayowahusu ikiwa ni pamoja na masuala ya chanjo ya UVIKO -19 na namna ya kujikinga na maradhi hayo.