UNYANYAPAA  WAPIGWA VITA

0
181

Serikali yaagiza hatua kali kwa wanaowanyanyapaa WAVIU
 
 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza mamlaka husika kuchukua hatua kali za kisheria kwa watu watakaobainika kuwanyanyapaa na kuwabagua watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU).
 
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo mkoani Mbeya wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani,  ambayo yamefanyika kitaifa mkoani humo.
 
 
 Amesema vitendo, kauli au mitazamo ya unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi havikubaliki, hivyo ni lazima watu wanaoendeleza unyanyapaa huo wachukuliwe hatua.
 
 
“Kumekuwa na madai kuwa watumishi wa afya wana tabia za unyanyapaa na kuvujisha siri za WAVIU wanapotoa huduma katika vituo vyetu vya tiba na matunzo kwa WAVIU, vitendo na tabia hizi ziripotiwe mara moja pindi vitakapotokea.” Ameagiza Waziri Mkuu Majaliwa
 
 
Ameongeza kuwa vitendo vya unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi vinakwaza na kurudisha nyuma mapambano dhidi ya Ukimwi nchini, kwa kuwa baadhi ya watu wanaoishi na VVU wanashindwa kutojitokeza na kupata huduma.
 
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, katika kudhibiti kuenea kwa maambukizi mapya ya Ukimwi Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kutekeleza mkakati wa nne wa Taifa wa kudhibiti Ukimwi kwa kushirikisha sekta zote nchini.
 
 
Amesema mkakati huo wa mwaka 2018/2019 hadi 2022/2023 umelenga kupunguza maambukizi mapya ya virusi vinavyosababisha ukimwi pamoja na vifo.
 
 
Kauli mbiu ya Kitaifa ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa mwaka huu ni zingatia usawa, tokomeza ukimwi, tokomeza magonjwa ya mlipuko.