Waziri mwenye dhamana ya Michezo nchini Innocent Bashungwa leo Disemba 1, 2021 amewaongoza watanzania kuishangilia Timu ya Tanzania (Tembo Warriors) ambayo imefuzu na kuwa timu ya kwanza miongoni mwa timu nne zinazoingia nusu fainali ya Soka ya Bara la Afrika kwa wenye ulemavu (CANAF 2021) na hivyo kupata tiketi ya kushiriki Mashindano ya Dunia ya mchezo huo yatakayofanyika nchini Uturuki 2022 baada ya kuichapa timu ya Cameroon mabao 5-0.
Timu ya Tanzania ambayo katika kipindi chote cha maandalizi imesimamiwa na Kamati Maalum ya Kitaifa chini ya Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassani Abbasi ilianza vizuri kutokana hamasa iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hasan.
Katika mechi zote za mashindano haya Tanzania imepoteza mechi moja tu ya Uganda mbayo ilifungwa goli 1-0, ambapo Tembo iliifunga timu ya Morocco 2-1 na Sierra Leone ambapo tembo ilishinda goli 1-0.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya mechi hii, Bashungwa amewahakikishia kwamba Serikali itaendelea kuiisaidia timu hiyo ili iendelee kufanya vizuri maandalizi ya Kombe la Dunia.
Aidha, Dkt Abbasi amesema kwa kuwa safari ya kuelekea kombe la dunia imekamilika kazi iliyobaki ni kuhakikisha kuwa kombe linabaki Tanzania.
Magoli mawili ya Tanzania yamefungwa na Alfan Kyanga dakika ya 2 na 15 , Ramadhan Chomole dakika ya 18, na Frank Ngailo dakika ya 36 na 44.
Mchezo huo pia umeshuhudiwa na Rais wa Mashindano hayo duniani Mateus Wildack.