Watumishi wa bandari kupata mafunzo Singapore

0
255

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema Serikali itashirikiana na uongozi wa bandari ya Singapore katika kutoa mafunzo kwa watumishi wa bandari za Tanzania.
 
 
Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo mara baada ya kutembelea bandari ya Singapore na kujionea namna inavyofanya kazi.
 
Amesema Tanzania pia itahakikisha watalaamu wa bandari kutoka Singapore wanakuja Tanzania ili kushirikiana na wenzao kufanya maboresho ya haraka hasa katika bandari ya Dar es Salaam.
 
 
Kwa mujibu wa Dkt. Mpango, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano umedhamiria kuifanya Tanzania  kuwa kituo kikuu cha biashara kwa kuweza kupitisha mizigo ya ndani ya nchi pamoja na nchi zote zinazoizunguka kwa kupitia bandari,  hivyo  ushirikiano na nchi ya Singapore katika kuboresha bandari zote za Tanzania Bara na Zanzibar utaongeza kasi katika utekelezaji wa mpango huo.
 
 
Katika ziara yake katika bandari hiyo ya Singapore, Makamu wa Rais ameshuhudia teknolojia mbalimbali zinazotumika katika kufanya kazi ikiwa ni pamoja na upakuaji na upakiaji makasha na mizigo, ukaguzi wa mizigo na ufuatiliaji makasha wakati wote yanapokuwa safarini.