Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kenya (DCI) George Kinoti amehukumiwa kifungo cha miezi minne jela kwa kukaidi agizo la Mahakama Kuu ya nchi hiyo lililomtaka kurudisha bunduki ya mfanyabiashara mmoja nchini humo.
Kinoti ametakiwa kujisalimisha ndani ya kipindi cha siku saba na endapo atapuuza agizo hilo, Mkurugenzi wa Mashtaka wa Kenya atalazimika kutoa hati ya kumkamata.
Mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu, DCI Kinoti alipewa muda wa siku 30 na Mahakama Kuu ya Kenya kurudisha bunduki na risasi zote zilizochukuliwa kutoka kwa mfanyabiashara huyo Jimi Wanjigi.
Kwa mara ya kwanza agizo hilo lilitolewa na Mahakama Kuu ya Kenya mwaka 2019 lakini Kinoti hakulitekeleza.