Mahakama kuu kusikiliza kesi ndogo ya Mbowe na wenzake

0
179

Mahakama Kuu Divisheni ya makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imepanga kusikiliza kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi ya Uhujumu yenye mashtaka ya kula njama na kutenda vitendo vya kigaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman MboweKuuwenzake watatu.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa utetezi Fredrick Kiwelo, pamoja na mawakili wenzake, kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Mohamed Ling’enywa.

Maelezo hayo ya onyo yametolewa leo na shahidi wa nane katika kesi hiyo, Mrakibu wa Polisi Jumanne Malangahe, ambaye aliomba mahakama hiyo ipokee maelezo hayo ili yatumike kama kielelezo katika kesi hiyo.

Katika ushahidi wake SP Malangahe amedai kuwa alichukua maelezo ya Ling’wenya , Agosti 7, 2020 katika kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salam.

Hata hivyo, upande wa utetezi wamepinga kielelezo hicho kisipikelekwe na Mahakama kwa kuwasilisha hoja mbalimbali zikiwemo za Ling’enywa kuchukuliwa maelezo yake kituo hicho Kikuu Cha Polisi Dar es Salama, pia alitishiwa na silaha wakati akiwa kituo cha Polisi Mbweni wakati akilazimishwa kusaini maelezo ambayo hakuyaandika.

Pia mawakili hao wamedai kuwa maelezo ya mtuhumiwa huyo yalichukuliwa nje ya muda unaoruhusiwa kisheria ambao ni masaa manne tangu kukamatwa kwa mtuhumiwa.

Wakili wa Serikali Robert Kidando amedai wamepitia mapingamizi hayo na kudai kuwa mapingamizi mawili kati ya matano yaliyotolewa na mawakili wa utetezi ndiyo yenye mashiko hivyo kuomba muda wa kuajiandaa na kesi ndogo ndani ya kesi kubwa.

Katika hatua nyingine Mahakama hiyo imepokea nyaraka ya shahidi wa nane SP Jumanne Malangahe ya kukamata mali kwa mtuhumiwa Adam Kasekwa nakupiga chini pingamizi la Upande wa Utetezi uliodai kwamba sheria iliyotumika kwenye ukamataji wa mali kwa mtuhumiwa Kasekwa haipo.

Jaji Joachim Tiganga amedai Mahakama inapokea nyaraka hiyo kwa sababu Upande wa utetezi hakuonyesha ni kwa namna gani ambavyo kukosewa kwa nyaraka hiyo kunaweza kuawaathiri wateja wao.

Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 10 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikiliza kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ambapo pande zote mbili za Jamhuri na Utetezi utatakiwa kuwasilisha mashahidi wake