Tanzania kutangaza miradi mikubwa Expo 2020 Dubai

0
5291

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania katika kuitangaza nchi kupitia
maonesho ya Biashara ya Kimataifa Dubai (Expo 2020 Dubai) yaliyofunguliwa mwezi huu na yanayotarajiwa kumalizika mwezi Machi mwaka 2022.

Rais Samia Suluhu Hassan atatakuwepo kwenye maonesho hayo katika tarehe maalum iliyopangwa ambayo ni 26 ya mwezi Februari mwaka 2022.

Akiwa katika maonesho hayo, Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mambo mengine ataeleza fursa za kibiashara na uwekezaji zilizopo Tanzania na uwepo wa miradi mikubwa ambayo itarahisisha biashara na uwekezaji.

Hayo yameelezwa mkoani Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa wizara ya Viwanda na Biashara Dotto James wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu namna Tanzania itakavyoshiriki katika maonesho hayo ya Biashara ya Kimataifa Dubai kwa kipindi cha miezi sita.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Dkt. Godwill Wanga amesema, maonesho hayo yatatoa nafasi kwa Tanzania kutangaza miradi mikubwa ya maendeleo pamoja na kutoa nafasi kwa Wawekezaji kufahamu mazingira na mipango ya Tanzania katika kufanikisha uwekezaji kutokana na kuwa na fursa nyingi.

Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dubai yanatarajiwa kufanyika kwa muda wa miezi sita na kushirikisha zaidi ya mataifa 190.

Tanzania imekuwa ikishiriki katika maonesho hayo tangu mwaka 1970.