TBC kushirikiana na Vyombo vingine vitatu kurusha maudhui ya miaka 60 ya Uhuru

0
2501

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Clouds Media Group, Wasafi Media na Mwananchi Communication Limited zimezindua nembo na ushirikiano utakaoviwezesha vyombo hivyo kurusha maudhui mbalimbali kuhusiana na maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru.

Wakuu wa Taasisi hizo wamefanya uzinduzi wa nembo maalum itakayotumika na vyombo vyote vinne vya habari kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru huku wakikubaliana kushirkiana katika maeneo mbalimbali ya kimaudhui.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Gabriel Nderumaki amesema, ushirikiano huo una lengo la kugusa makundi yote katika jamii na ndio maana wameamua kuungana ili kuwaleta pamoja Watanzania wa makundi yote.

Mkurungenzi Mkuu wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga amesema, katika maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru, wao kama Clouds wameona ni muhimu kuungana na wengine ili kuwa na ujumbe wa pamoja kwa Watanzania hasa katika kipindi hiki.

Mkurugenzi wa Vipindi wa Wasafi Media, Nelson Kisanga amesema, kundi la vijana litawakilishwa vyema kupitia maudhui yanayoandaliwa wakati huu ili na wao wafahamu historia ya uhuru wa Taifa kupitia matamasha na michezo iliyoandaliwa kwa pamoja nyimbo 60 kutoka kwa wasanii 60 wa vizazi vilivyokulia ndani ya Uhuru zitarekodiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communication Limited, Bakari Machumu amesema, Mwananchi wameanza kufanya midahalo katika maeneo nane na wameamua kuungana na vyombo vingine ili kuwa na ajenda ya pamoja katika maadhimisho hayo ya Uhuru.