Tanzania tajiri wa nishati jadidifu

0
196

Wakati dunia ikikaribia kukutana nchini Uingereza kwa ajili ya mkutano mkubwa wa jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, Tanzania imetajwa kuwa na nguvu kubwa ya kuzalisha nishati jadidifu ambayo ni muhimu katika kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi na pia kuongeza upatikanaji wa nishati mbalimbali hasa umeme kwa ajili ya uzalishaji katika viwanda.

Hayo yamezungumzwa na mshauri wa Jiolojia, John-Bosco Tindyebwa katika mkutano uliondaliwa na shirika la HakiMadini kwa ajili ya kuelimisha waandishi wa habari kuhusu nishati jadidifu na nguvu ambayo taifa la Tanzania inayo katika upatikanaji wa nishati hiyo.

Maeneo ambayo Tanzania inaweza kutumia kuzalisha nishati hiyo ni pamoja na jua, upepo, mawimbi ya bahari, takataka zinazotokana na matumizi ya nyumbani ambavyo vyote vinapatikana kwa wingi hapa nchini.

Mtaalamu huo amesisita waandishi wa habari kuelimisha jamii zaidi kuhusu utajiri wa asili ambao Tanzania inayo ambao unaweza kutumika kubadilisha njia za uzalishaji wa nishati na kukuza uzalishaji na maisha ya watu wa kawaida.

“Ukiangalia mikoa hasa ya Nyanda za Kati na Juu kama Singida, Dodoma, Simiyu, Shinyanga, Mbeya, Tabora zinaweza kuzalisha nishati jadidifu kutokana na vyanzo kama jua na upepo na kuongeza nguvu katika gridi ya taifa. Tuelimishe jamii ili hata kizazi kijacho kifanye vizuri zaidi katika kukutumia utajiri huu,” amesema mshauri huo wa jiolojia katika mafunzo hayo

Mafunzo hayo yanadhamiria kutoa elimu endelevu kwa waandishi wa habari ili kutoa chachu kwa viongozi husika na jamii kujua na kubuni njia za uzalishaji wa nishati jadidifu ambayo zaidi ya kurahisisha maisha ya Mtanzania lakini pia inaweza kutumika kama chanzo cha biashara.