Kagera yaona mwezi mbele ya Mtibwa Sugar

0
408

Kagera Sugar ya mkoani Kagera imepanda hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama tano baada ya kupata ushindi wa kwanza katika michezo minne iliyoshuka dimbani.

Katika mchezo wa leo ambao iliwakaribisha wazalisha sukari wenzao wa Morogoro, Mtibwa Sugar, Wana Nkurukumbi hao walipata goli pekee na la ushindi dakika ya 39 kupitia kwa Dickson Mhilu.

Kagera Sugar imepoteza mchezo mmoja, huku ikitoka sare mbili na kupata ushindi mara mmoja.

Kwa upande wa Mtibwa Sugar imeporomoka hadi nafasi ya 12 kutoka nafasi ya 10 iliyokuwepo kabla ya mchezo huo.

Wakata miwa hao wa Morogoro wana alama mbili baada ya kushuka dimbani mara nne, wakiwa wamepata droo mbili na kupoteza michezo miwili.

Ligi hiyo itaendelea tena Oktoba 23 ambapo Namungo FC itaikaribisha KMC katika Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi, mchezo utakaorushwa na TBC FM kuanzia saa 8:00 mchana.

Mchezo mwingine Geita Gold FC itaikaribisha Mbeya City katika Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita, mchezo utakaorushwa na TBC Taifa kuanzia saa 10:00 jiioni.