NARCO yakodisha asimilia 75 ya eneo lake

0
177

Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imekodisha maeneo kwa wafugaji, hali iliyochangia kupunguza migogoro baina ya wafugaji hao na watumiaji wengine wa ardhi.
 
Kauli hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya NARCO Paul Kimiti wakati wa kikao cha mwisho cha bodi hiyo ambayo imemaliza muda wake baada ya kukaa madarakani kwa takribani miaka mitatu.
 
Amesema bodi hiyo imefanikiwa kusimamia na kuhakikisha wafugaji nchini wanapatiwa maeneo kwa mikataba katika ranchi za Taifa,  ili waweze kufuga vizuri na kukuza sekta ya mifugo.
 
“Tumegawa maeneo ya ranchi takriban asilimia 75 na kubakiza asilimia 25 kwa kuwa Wafugaji nchini wamekuwa na mifugo mingi na wanahitaji maeneo kwa ajili ya kufuga mifugo yao.” amesema Kimiti
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NARCO Profesa Peter Msoffe amesema bodi ya wakurugenzi iliyomaliza muda wake imeweka misingi imara katika kufuatilia ukubwa wa maeneo ya ranchi, madeni na mashauri mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa yameiwezesha NARCO kupata mafanikio zaidi.
 
Ameongeza kuwa bodi hiyo imekuwa ikitoa maelekezo kwa NARCO kuhakikisha inakaa na wawekezaji ambao wamepatiwa vitalu na kuona namna ya kuboresha mikataba, ili iweze kuzinufaisha pande zote mbili.