Mkandarasi aagizwa kukamilisha ujenzi wa mizani

0
5747

Mkuu wa mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marko Gaguti ametoa muda wa siku saba kwa mkandarasi anayejenga ghala la kuhifadhia korosho katika kijiji cha Mtimbwilimbwi halmashauri ya mji wa Nanyamba, kukamilisha ujenzi wa mizani ya kupimia zao hilo.

Brigedia Jenerali Gaguti ametoa muda huo wakati akiwa kwenye ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo akiwa ameongozana na kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Mtwara.

Amesema pamoja na kutoa agizo hilo atarudi katika kijiji cha Mtimbwilimbwi ndani ya siku mbili kuangalia hatua za ujenzi wa mizani hiyo na kama haujakamilika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mkandarasi huyo.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa ghala hilo, Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU Biadia Matipa amesema ujenzi wa ghala hilo umefikia asilimia 90 na kutumia zaidi ya shilingi milioni 797.43 na litakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 500 hadi 700 za mazao kwa wakati mmoja.