Rais Samia : Sijali ukabila, najali kazi

0
141

Rais Samia Suluhu Hassan amesema katika utendaji wake wa kazi hajali ukabila, bali anachojali ni kazi anayofanya mtu.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha Viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni.

Amesema wanaodhani kuwa anafanya kazi ya kuteua Viongozi kwa kuangalia wanatoka eneo fulani ama kabila fulani, waondoe dhana hiyo potofu.

Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa anachofanya yeye ni.kumteua Kiongozi kutoka eneo ama kabila lolote anapoona kuna mtu anafaa na pia amekuwa akitengua kwa kuangalia ni jambo gani amekosea kiongozi huyo na si vinginevyo.

Viongozi walioapishwa hii leo katika hafla hiyo ni pamoja na  Sofia Mjema aliyeapishwa kuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga na Jaji Omar Othman Makungu aliyeapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Mwingine aliyeapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni Jaji Mustapha Siyani ambaye ameapishwa kuwa Jaji Kiongozi.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma.