Mark Zuckerberg apata hasara trilioni 13

0
4852

Utajiri wa mmiliki wa Kampuni ya Facebook, Mark Zuckerberg imeshuka kwa shilingi trilioni 13.8 kwa saa chache ambazo mtandao huo na kampuni tanzu za WhatsApp na Instagram hazikuwa hewa, Bloomberg imeripoti.

Utajiri wake binafsi sasa imeshuka kufikia shilingi trilioni 279, kiasi kinachomfanya kuwa mtu wa tano kwa utajiri duniani kutoka nafasi ya tatu katika orodha ya Bloomberg, huku Forbes ikimtaja kuwa tajiri namba sita.

Hali ya kukosekana kwa mitandao hiyo kwa takribani saa sita kunatajwa kuwa ndio muda mrefu zaidi, kwa tatizo hilo kuwepo.

Tatizo la upatikanaji wa Facebook limekuja wakati kampuni hiyo ikishutumiwa pia kuweka mbele biashara kuliko usalama wa watumiaji wa mtandao huo. Frances Haugen, ambaye alikuwa mfanyakazi wa kampuni hiyo amejitokeza hadharani na kuishutumu Facebook kwa kusambaza kwa makusudi taarifa za uongo.

“Kulikuwa na mkanganyiko mara kwa mara kuhusu kipi ni kizuri kwa Facebook na kipi kizuri kwa umma, na mara kwa mara Facebook ilichagua kuweka mbele maslahi yake, kama kupata faida zaidi,” amesema Haugen.