Tanzania kupeleka sita mashindano ya urembo Brazil

0
1850

Tanzania imepata nafasi ya kupeleka washiriki sita kwenye Fainali za Urembo, Mitindo na Utanashati kwa Viziwi ya ngazi ya Dunia yatakayofanyika Aprili 2022 nchini Brazil kufuatia ushindi wa kishindo wa washiriki wake wawili waliofanya vizuri kwenye Fainali za Afrika zilizomalizika Jijini Dar es Salaam Oktoba Mosi mwaka huu. 

Katika shindano hilo la kwanza kufanyika Afrika na Tanzania kuwa mwenyeji, washiriki wa Tanzania walioshinda ni Khadija Kanyama aliyeshika nafasi ya pili Afrika (Kundi la Miss Deaf Afrika 2021) na Carloyne Mwakasaka (Kundi la Miss Deaf Africa – Fashion) aliyekuwa mshindi wa kwanza. 

Kutokana na ushindi huo Kamati ya Kimataifa ya Mashindano hayo imetoa taarifa ya washiriki wengine wanne kutoka Tanzania ambao sasa nao wamekidhi vigezo vya kushiriki mashindano hayo kwa ngazi ya dunia kuwa ni Surath Mwanis, Rajani Ali na Russo Songoro upande wa Mavazi na Mitindo huku Joyce Denis akipata nafasi ya kushiriki katika eneo la urembo.

Jumla ya washiriki 8 wa Tanzania waliungana na washiriki wengine zaidi ya 30 kutoka nchi nyingine 12 za Afrika. 

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Mashindano hayo kidunia ambaye pia alikuwa Jaji Mkuu wa shindano hilo la Dar es Salam, Artur Dzerbis, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuandaa mashindano haya katika kiwango cha juu kwa kuwa ndio yamefanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika na kueleza kuwa Kamati ya Dunia imeridhishwa na kiwango hicho. Wakati huo huo, Makamu huyo wa Rais amesema Kamati yake imepokea maombi ya Serikali ya Tanzania yaliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, ya utayari wa nchi yetu kuendelea kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa ngazi ya Bara la Afrika kwa miaka mitatu zaidi.

Amesema ombi hilo litawasilishwa kwenye Kamati ya Kimataifa na kutolewa uamuzi kwani Tanzania imeonesha uzoefu na uwezo mkubwa kupitia shindano hilo la kwanza. Kwa upande wake, Dkt. Abbasi, amewaomba wadau mbalimbali kuwasaidia washiriki hao wa Tanzania ili kuwawezesha kujiandaa vyema na kufanya vizuri zaidi huko Brazil ili kuiletea sifa nchi yetu.Jana Oktoba 02, 2021, washiriki wote kutoka nchi 12 za Afrika na majaji kutoka Marekani na Ufaransa walipata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii wa kihistoria na utamaduni kwa kutembelea kwenye Ofisi za Program ya Historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika jijini Dar es Salaam na kisha maeneo mbalimbali ya Bagamoyo mkoani Pwani.