Taarifa rasmi ya serikali kuhusu uraia wa Kibu Denis

0
1266

Serikali imempatia uraia wa Tanzania mshambuliaji wa Simba SC, Kibu Denis Prosper ambaye siku za karibuni alikuwa gumzo baada ya kuibuka kwa utata kwenye uraia wake.

Akizungumza na TBC kwa njia ya simu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema nyota huyo aliyejiunga na Simba akitokea timu ya Mbeya City ya jijini Mbeya amepewa uraia tangu Septemba 30 mwaka huu.

Waziri Simbachawene amesema amempa uraia kwa mujibu wa Sheria ya Uraia, Sura ya 357 (Rejeo la 2002), baada ya kupokea ombi lililopelekwa kwake na TFF kupitia Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo.

Alipoulizwa kuhusu uraia wa asili wa Kibu Denis amesema mchezaji huyo alikuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), lakini amekuwepo nchini Tanzania tangu mwaka 1998, akiwa na umri wa miaka sita, baada ya wazazi wake kukimbia machafuko ya kisiasa nchini humo.

Ameongeza kuwa mchezaji huyo amekuwa na nyaraka zinazoonesha ni raia wa Tanzania, ikiwemo kitambulisho cha uraia, kwani yeye alikuwa anajijua ni Mtanzania kutokana na kuingia nchini akiwa na umri mdogo, na hana historia yoyote na nchi yake ya asili zaidi ya kukulia Tanzania.

Sakata la uraia wa Kibu Denis lilianza baada ya kutoitwa kwenye timu ya taifa ya mpira wa miguu (Taifa Stars) iliyokuwa inajiandaa na michezo ya kufuzu kwa fainali za FIFA za Kombe la Dunia, dhidi ya timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Madagascar, ambao kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen alilalamikia kitendo cha kumkosa mchezo huyo ikiwa ni wiki chache zimepita baada ya kucheza na kuonesha kiwango kizuri kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi.