Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia SIDO kushirikiana Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Balozi za Tanzania nje ya nchi katika kupata teknolojia rafiki, mitaji, kutafuta masoko ili kuendeleza viwanda vidogo na vya kati hapa nchini, kukuza ajira na kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi.
Dkt. Mpango ameyasema hayo alipokuwa akifungua rasmi Maonesho ya tatu (3) ya SIDO Kitaifa yanayolenga kutoa fursa kwa wajasiriamali kupanua wigo wa masoko ya bidhaa, kuongeza uzalishaji, kubadilishana uzoefu na ujuzi na kuboresha bidhaa kulingana na mahitaji ya soko ambayo yameanza tarehe 21 hadi 31 Septemba 2021 katika viwanja vya Umoja Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.
Akizungumzia Kauli Mbiu ya Maonesho hayo ya SIDO ya mwaka huu inayosema “Pamoja Tujenge Viwanda kwa Uchumi na Ajira Endelevu”, Dkt. Mpango ameagiza kuwa maonesho au maadhimisho mbalimbali yanayofanyika nchini yafanyiwe tathmini ya utekelezaji wa Kauli mbiu husika ya kipindi/mwaka uliotangulia.
Aidha, Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kufanya tathimini kuhusu utekelezaji wa malengo ya kuanzishwa kwa SIDO pamoja na kupitia mahitaji ya bajeti yake na kutoa mapendekezo ya mikakati mipya ya kuiboresha na kuitafutia vyanzo vingine vya mapato ili kuiwezesha Tanzania kukidhi mahitaji ya uchumi wa kati.
Vile vile, ameelekeza SIDO na Taasisi zote za umma na binafsi zinazojihusisha na maendeleo na teknolojia ya viwandani zichukue hatua za dhati na kujiwekea malengo ya kulinyanyua Taifa katika utengenezaji wa mashine mbalimbali za kuchakata na kuongeza thamani mazao ya kilimo kwa kutumia teknolojia rahisi na nafuu.
Makamu wa Rais pia amezitaka Taasisi za kifedha kubuni na kutoa Mikopo kwa wajasiriamali wadogo yenye riba nafuu, kutoa elimu kuhusu ubora wa miradi, usimamizi wa miradi na matumizi adili ya mikopo inayotolewa ili kuongeza uzalishaji, ajira na kupunguza umaskini huku akiwataka wajasiriamali hao kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Kwa upande wa SIDO, Dkt. Mpango ameliagiza Shirika hilo kuendelea kuhamasisha na kutoa mafunzo kwa wananchi ili waweze kuingia katika shughuli zinazotumia teknolojia rahisi na nafuu hususan katika uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao na bidhaa mbalimbali kwa kutumia mashine, vipuri na bidhaa zinazozalishwa kwa gharama nafuu, zinazokidhi viwango na kuhimili ushindani wa soko.
Aidha, Dkt.Mpango ameitaka SIDO kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili kutunisha Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wajasiriamali (NEDF) ili kuwapatia wajasiliamali mikopo yenye masharti nafuu, kutoa elimu, ujuzi, taarifa, mtaji, kuwalea na kuwakuza pamoja na kutangaza fursa hizi kwa wananchi.
Dkt. Mpango pia ametoa wito kwa wananchi kuungana na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha kuondoa changamoto ya upungufu wa mafuta ya kula nchini kwa kuongeza uwekezaji katika kilimo na uchakataji wa mbegu za mafuta huku akiagiza uwekezaji wa Kiwanda kikubwa cha kukamua na kutakasa Mafuta ya Mawese kuanzishwa Mkoani Kigoma kabla ya Mwaka 2025.
Katika kuboresha mazingira ya Biashara na uwekezaji, Dkt. Mpango amewaelekeza Wakuu wa Mikoa wote nchini kupitia Kamati za Maendeleo za Mikoa kuongeza viwanda vidogo kila Wilaya vinavyochakata mazao ya kilimo. Pia amezitaka Wizara za Kilimo, Viwanda na Biashara, Elimu, Teknolojia & Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Fedha na Mipango kutoa kipaumbele kwa utafiti na maendeleo (R & D) ili kukuza uchumi wa viwanda nchini.