Rais Samia awaomba wananchi kutodharau mabadiliko ya Tabia Nchi

0
169

Rais Samia Suluhu Hassan, amewaomba wananchi kuto kupuuzia hali ya kupanda kwa joto kwa kuwa hali hiyo husababisha ukame ambao huleta athari kubwa kwenye sekta zinazotegemea maliasili kama vile kilimo,uvuvi na misitu.

Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo jana kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa, uliojadili athari za mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoikumba dunia na kusisitiza umuhimu wa kutopuuzia juhudi za kukabiliana na janga hilo, ili kuepuka athari zinazotokea kutokana na kutokea kwa mabadiliko hayo yaayoweza kuiingiza nchi kwenye janga kubwa la njaa kutokana na ukame.

Wakati huo huo Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Comoro,Azali Asoumani na Makamu wa Rais wa Sudan Kusini,Rebecca Nyandeng Garang ambapo kubwa kwenye mazungumzo yao wamezungumzia kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na mataifa hayo.

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Filippo Grandi, ambapo viongozi hao wamezungumzia kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Shirika hilo hususan katika kusaidia wakimbizi walioko nchini Tanzania.

Filippo Grandi ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kubeba mzigo mkubwa wa wakimbizi kwa takribani miongo sita sasa ambapo pia amependekeza kuwepo na mkutano katika ngazi ya wataalam baina ya UNHCR, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuondoa changamoto katika kuwahudumia wakimbizi.

Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kikao hicho kufanyika mara moja ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji.