Naibu Waziri Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amewahakikishia wawekezaji wote nchini kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan haitachoka kusikiliza kero mbalimbali za wawekezaji nchini ili kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia Viwanda.
Ameyasema hayo leo Septemba 15, 2021 alipofanya ziara katika kiwanda cha kutengeza saruji cha Nyati kilichopo Kimbiji, Kigamboni mkoani Dar es salaam ambapo amekutana na Mwendeshaji Mkuu wa Mitambo wa kiwanda hicho ndugu Biswajeet Mallik na kufanya nae mazungumzo.
Kigahe amesema kuwa nia ya serikali ni kuona viwanda vyote nchini vinazalisha kwa wingi wakati wote ili kuendelea kukuza ajira kwa Watanzania, lakini pia malighafi zinazotengenezea saruji zinapatikana ndani ya nchi hivyo hakuna sababu kwa wasambazaji na wauzaji wa saruji kupandisha bei kwani anayeathirika ni mlaji wa mwisho.
Kiwanda cha Nyati kina uwezo uliosimikwa wa kuzalisha tani elfu sita (6000) kwa mwaka ambapo kwa sasa kinazalisha kwa asilimia 100. Pia kiwanda kimeajiri wafanyakazi wa moja kwa moja wapatao 350 na ajira nyingine zisizo za moja kwa moja kama watoa huduma za chakula, wasafirishaji na wauzaji.
Aidha, katika ziara hiyo Naibu Waziri Kigahe ametembelea Kituo cha Biashara, Ugavi na Viwanda nchini (Kurasini Industrial, Trade and Logistic Centre) na kutoa maagizo kwa wananchi ambao hawajahama kufanya hivyo ifikapo Oktoba 2021 ili Serikali iendeleze eneo hilo.