Kina cha Maji Mto Ruvu chapungua

0
146

Mamlaka ya usimamizi wa bonde la mto Ruvu na wami (Wami-Ruvu) imesema huenda Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ikakumbwa na uhaba wa huduma ya maji kutokana na kupungua kwa kina cha maji katika mto Ruvu.

Hali hiyo inatokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu katika mto huo hali inayofanya kina cha maji kuendelea kupungua kwa kasi kubwa.

Kaimu Mkurugenzi Bodi ya maji bonde la Wami – Ruvu Elibariki Mmasi, amefanya ukaguzi katika mto huo na kusema kuwa kina cha maji kimezidi kupungua tofauti na ilivyokuwa Septemba mwaka jana.

Mmasi ameongeza kuwa Shughuli za Kibinadamu pamoja na kutokuwepo kwa mvua za Kutosha ni Sababu ambazo zinachangia pakubwa kutokea kwa hali hiyo.

Kufuatia hali hiyo Kaimu mkurugenzi huyo wa Bodi ya maji Wami Ruvu ametoa rai kwa Wananchi hususani wa Dar es Salaam na Pwani kutumia maji kwa uangalifu ili kukabiliana Changamoto hiyo.

Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu ni Taasisi ya Serikali inayoshughulika na uhifadhi, utunzaji na uendelezaji wa vyanzo vya maji hapa nchini.