Waziri Mkuu ataka makao makuu yajengwe Mahembe

0
233

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Kigoma yajengwe katika kata ya Mahembe kama ilivyopendekezwa awali na Baraza la Madiwani na si katika eneo la Kamala linalopendekezwa na watalaam hivi sasa.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo baada ya kusimamishwa na Wakazi wa kata hiyo akiwa njiani kwenda kukagua shamba la michikichi katika gereza la Kwitanga ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Kigoma.

Wakazi hao wa kata ya Mahembe wamemweleza Waziri Mkuu Majaliwa kuwa wamesikitishwa na hatua ya kubadilishwa kwa mapendekezo hayo ya awali yalitolewa na Madiwani.

Waziri Mkuu ameagiza kama sababu ni eneo la kata ya Mahembe kutofaa kwa ujenzi wa majengo ya ghorofa, basi ramani ibadilishwe ili yajengwe majengo ya kawaida.

Aidha Waziri Mkuu Majaliwa ameiomba   Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusimamia jambo hilo.

Amesema Serikali inathamini na kuheshimu uamuzi ya Wananchi ambao tayari wamejitolea ardhi yao yenye ukubwa wa hekari 25 kwa ajili ya ujenzi huo wa  makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Kigoma.