Mbowe na wenzake wasomewa mashtaka upya

0
141

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe na wenzake watatu, wamesomewa upya mashtaka yao sita mbele ya Jaji Mustapher Siyani.

Mbowe na wenzake wamefikishwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi iliyopo mkoani Dar es Salaam, ambapo kwa mara ya kwanza leo wataruhusiwa na mahakama hiyo kujibu tuhuma zinazowakabili kwa kusema ndio wanakubaliana nazo au hapana hawakubaliana na tuhuma hizo.

Mbowe na wenzake wamefikishwa katika Mahakama hiyo mapema asubuhi ya leo wakiwa chini wa ulinzi mkali wa Jeshi la Magereza pamoja na Polisi.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwamo la kukutwa na sare na vifaa vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), makosa ambayo wnadaiwa kuyatenda kati ya Agosti Mosi na 5 mwaka 2020 katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Arusha, Morogoro, Moshi na Dar es Salam.

Washtakiwa hao wanasomewa hoja za awali na Wakili wa Serikali Tulimanywa Majigo.

Katika kesi hiyo Mwenyekiti huyo wa CHADEMA anatetewa na Wakili Peter Kibatala akisaidiana na jopo la Mawakili wa kujitegemea.