Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya watu wanaotoa maneno yasiyofaa kuhusu chanjo dhidi ya UVIKO 19, kuacha kufanya hivyo.
Akizungumza mkoani Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya mifugo nchini, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali imejiridhisha na usalama wa chanjo hiyo, ndio maana imeruruhusu itolewe ili watu wajikinge na ugonjwa huo.
Amesema tofauti na ilivyotarajiwa, chanjo hiyo hapa nchini imezusha maneno mengi, jambo ambalo halipendezi.
Waziri Mkuu amesema Viongozi wa Serikali tangu mwaka 2020 ugonjwa wa UVIKO 19 ulipoingia nchini kwa mara ya kwanza walisema hawataleta chanjo mpaka wajiridhishe, na tayari wamejiridhisha na kuruhusu iingie nchini.
Amewataka Watanzania wote kutoyajali maneno hayo na waendelee kujitokeza kupata chanjo hiyo, ili wajikinge na ugonjwa huo hatari.